Tafakuri ya 7, Āyāt 26: 87 – 89: Moyo Uliosalimika

وَلَا تُخْزِنِي يَوْمَ يُبْعَثُونَ * يَوْمَ لَا يَنْفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ* إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ
Wala usinihizi siku watakapofufuliwa. Siku ambayo haitafaa mali wala wana. Isipokuwa mwenye kuja kwa Mwenyezi Mungu na moyo uliosalimika.
(Sūratush Shu‘arā, Na. 26, Āyāt 87-89)

Du’a hii ni sehemu ya mtiririko wa du’a ya Nabii Ibrahim (a). Nabii huyo anamuomba Mwenyezi Mungu amuokoe kutokana na huzuni katika ile siku ambayo mali za kidunia hazitakuwa na faida yoyote. Bidhaa pekee itakayomfaa vizuri zaidi yule aliyenayo katika siku ile itakuwa ni umiliki wa moyo uliosalimika. Maneno ya Kiarabu yaliyotumika katika aya hii ni “Qalbun Salīm.” Moyo uliosalimika hapa umeelezewa kama moyo ulio huru kutokana na maradhi na mapungufu, moyo ambao umetakasika na mnyofu, muaminifu. Kutokea humo huchomoza mawazo mema, maneno mazuri ya kupendeza, na matendo ya kiadilifu. Msingi wake ni wema, wenye mizizi katika mapenzi na Muumba Wake. Imam Ja’far al-Sadiq (a) wakati akiielezea aya hii anasema: “Qalbun Saliim ni moyo ambao unakutana na Mola Wake wakati ukiwa hauna yeyote zaidi ndani yake isipokuwa Yeye tu, swt.

Kama ulivyo mwili wa mwanadamu, moyo wa mwanadamu pia hupatwa na afya na maradhi. Wakati moyo unapokuwa salama na wenye afya njema, huwa tunajawa na utulivu na utambuzi wa wajibu wetu. Wakati moyo unapougua maradhi hauwezi kutekeleza kazi zake vizuri. Maisha hupoteza maana yake kwa vile ule moyo unaougua utayaona mambo yote kwa mtazamo wenye maradhi. Ugonjwa wa moyo ni janga ambalo lina athari kubwa sana katika matokeo ya baadae ya binadamu.

Imam Ali (a) anasema: “Kutoka kwenye mateso ni umasikini, na baya zaidi kuliko umasikini ni maradhi ya mwili, na baya zaidi kuliko maradhi ya mwili ni ugonjwa wa moyo. Kwa hakika miongoni mwa neema ni riziki yenye wasaa wa kutosha, na bora kuliko hilo ni afya ya mwili, na bora zaidi kuliko hilo ni afya ya moyo. Katika Qur’ani Tukufu, neno maradha(kwa maana ya magonjwa) linatokeza mara ishirini na nne, ambazo kutoka humo, zaidi ya nusu zinazungumzia maradhi ya moyo.

Kama vile ambavyo mwili wenye maradhi unavyoweza kushindwa kufanya kazi kama hautapata uangalizi wa kutosha, moyo unaougua pia unaweza kufa kama haukushughulikiwa. Kifo cha moyo ni hatari zaidi  kuliko kifo cha mwili. Katika Nahjul-Balāgha, Imam Ali (a) anawaelezea watu wachamungu na anasema: “Wao wanawaona watu wa dunia hii wakikikuza kifo cha miili, lakini wanajihusisha zaidi kuhusu kifo cha nyoyo za waliohai. Matokeo ya maradhi ya moyo ni kupotea kwa furaha ya kiroho katika ibada. Hakuna raha katika dhikiri na Du‘ā, hakuna uchangamfu wa moyo, hakuna kwenda mbele katika dini, na hakuna mhemko katika kuwa na uwezo wa kuongea na Mola. Huu ni ugonjwa unaodhoofisha ambao unazuia maendeleo zaidi ya kiroho. Hadithi kutoka kwa Nabii Isā (a) inasema:

“Kama vile mtu mgonjwa asivyoona raha ya chakula kitamu, moyo wenye maradhi hauoni furaha katika ibada ya Mwenyezi Mungu.”

Ni wajibu wa waumini kutunza afya za nyoyo zao. Tunahitaji kuzichunguza hali za mioyo yetu. Je, tunangojea kwa shauku kumuabudu Mwenyezi Mungu, kumkumbuka Yeye, kuongea Naye? Je tunachelewa kulala, au tunaamka mapema, ili kuwa miongoni mwa wale wanaotafuta msamaha wakati dunia ikiwa imelala na kutojali kitu? Je, tunalia kwa kumkumbuka Yeye? Kama tukijikuta wenyewe hatuathiriki na tusiostuka kwenye ukumbusho wa Mwenyezi Mungu, basi tunajua kwamba tumeumia.

Vyanzo: Āyatullāh Makārim Shirāzī, al-Amthāl fī Tafsīr Kitaballāh.
Aghā Muhsin Qarā’atī Kashānī, Tafsīr Nūr

Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo