Tafakuri ya Kwanza, Āyat 16:97: Maisha ya kupendeza

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِنْ ذَكَرٍ أَوْ أُنثَى وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُمْ بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ
(97/النحل)

Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya.
(Sūratun Nahl: 16:97)

Aya hii ni ahadi nzuri kwa muumini, ya matokeo ya matendo mema yanayoanzia kwenye imani juu ya Mwenyezi Mungu. Mwenye kufanya matendo mema atapata malipo katika dunia hii na katika Akhera. Mwelekeo wa kutumainisha na wa chanya wa aya hii unawasukuma waumini kuzidisha shughuli zao na kujitahidi kuongeza matendo yao mema.

Katika dunia hii, muumini atalipwa kupitia uhuishaji pamoja na maisha mazuri. Angalia kwamba Mwenyezi Mungu hasemi kwamba maisha yake yatakuwa mazuri, bali atapewa uhuisho, namna mpya ya maisha ambayo itakuwa nzuri na ya kupendeza. Ni maisha hayo hayo ambayo kwa sasa yamenururishwa kwa mwanga na nguvu ya ndani iliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu. Muumini anazawadiwa fursa za kupata kile ambacho vinginevyo kingekuwa hakiwezekani kupatikana.

Kitabu Al-Amthāl fī Tafsīr Kitābi-llāh kinatoa maelezo yafuatayo ya maisha mazuri na ya kupendeza ambayo muumini atalipwa kwayo:

a)  Maisha ambayo yana amani na kuridhisha.
b)  Maisha ambayo yana upatanifu, ushirikiano na upendo
c)  Maisha yasiyo na hofu wala huzuni. Hii ndio hali bora ya watu wa Peponi.   Inaweza kupatikana kwa kiasi fulani katika dunia hii wakati mtu anapokuwa haruhusu hali ya mambo ikamuathiri (au kumyumbisha). (Q 57:23)
d)  Maisha ambayo yanahangaikia kuelekea kwenye ukamilifu.(Q 48:29)
e) Muumini anayatazama maisha kwa mtazamo sahihi, kupitia Nuru ya Mwenyezi Mungu (Q 39:22)
f) Malaika wanamtakia rehma na kumuombea msamaha juu yake. (Q 40:7).

Huko Akhera Mwenyezi Mungu atawaliwalipa thawabu wale wanaotenda matendo mema kwa ubora wa kile walichokuwa wakikitenda. Kwa mujibu wa Al-Amthal fi Tafsir Kitabi-llah hii ina maana kwamba Mwenyezi Mungu atachukua thamani ya vitendo bora vya muumini, na kisha kulipa matendo mema yote mengine kwa thamani ileile ya ubora. Mfano wake katika dunia hii ni kama ule wa mnunuzi ambaye anataka kununua vitu vya thamani tofauti. Anachukua kile chenye bei ya juu zaidi na kulipia vitu vyote vingine kwa kulingana na thamani ileile. Hakuna binadamu ambaye angeweza kufanya hivyo kwa sababu kila mtu anaangalia manufaa na faida yake binafsi, sio faida ya yule mtu mwingine. Ni Muumba Peke Yake ambaye anawapenda sana viumbe Wake, kiasi kwamba anawaruhusu kufaidika mno. Hii ndio maana katika Sahīfa Sajjādiyyah, Imam Zaynul ‘Abidīn (a) anasema:

“Ni Wewe ambaye umeongeza bei dhidi Yako Mwenyewe kwa manufaa ya waja Wako, ukipendelea faida yao katika biashara na Wewe, furaha yao kupitia kukufikia Wewe na nyongeza yao kwa sababu Yako…..” (Du‘ā ya 45)

Aya hii pia inaonyesha jinsi wanaume na wanawake walivyo sawa mbele ya Mwenyezi Mungu. Wanaume na wanawake wamefanywa kuwa tofauti na Muumba. Wamepewa majukumu na wajibu tofauti katika dunia hii. Lakini hali zao za kiroho mbele ya Mwenyezi Mungu hazitegemei juu ya jinsia zao bali juu ya vitendo vyao. Wote wana fursa ya nafasi sawa ya kuweza kupata cheo cha hali ya juu kupitia imani zao na vitendo vyao.

Chanzo:
Āyatullāh Nāsir Makārim Shirāzī – Tafsir al-Amthal
Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo.