Tafakuri ya 6, Āyat 10:12 Mwitikio wa Binadamu Kwenye Hali ya Mambo

وَإِذَا مَسَّ الْإِنسَانَ الضُّرُّ‌ دَعَانَا لِجَنبِهِ أَوْ قَاعِدًا أَوْ قَائِمًا فَلَمَّا كَشَفْنَا عَنْهُ ضُرَّ‌هُ
مَرَّ‌ كَأَن لَّمْ يَدْعُنَا إِلَىٰ ضُرٍّ‌ مَّسَّهُ ۚ كَذَٰلِكَ زُيِّنَ لِلْمُسْرِ‌فِينَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

Na dhara inapomgusa mtu hutuomba naye ameegesha ubavu wake, au katika hali ya kukaa, au katika hali ya kusimama. Lakini tunapomwondolea dhara yake, huendelea kama kwamba hakupata kutuomba tumuondolee dhara iliyomgusa. Namna hii wamepambiwa  wapetukao mipaka yale waliyokuwa wakiyatenda.
(Sūratu Yūnus, Na.10, Āyat12)

Binadamu wanaweza kuwa na kigeugeu sana, wakati mmoja  wote wazuri kabisa na wema, na wakati mwingine wakawa na mioyo migumu na wasiojitambua. Kuyumba na kubabaika huku kati ya watu kunasababishwa na mwitikio wa ndani kwenye hali tofauti za nje. Wakati mwanadamu anapopitiwa na nyakati ngumu, anakuwa na haja ambazo hazijakidhiwa. Mahitaji haya yasiyotimizwa yanasababisha uwazi katika moyo. Unaleta fedheha kwani mwanadamu huyo anatambua kwa uchungu kabisa juu ya udhaifu wake mwenyewe na kukosa thamani. Shida na machungu anayoyapitia yako kama moto ambao unayeyusha moyo wake. Mapazia yaliyotengenezwa na kuipenda dunia, dhambi, uambatanishaji na kadhalika vinaondolewa, kukidhihirika silika zake za asili, za ndani kabisa. Anatafuta msaada kwa Mwenyezi Mungu na anamkumbuka kwa mfululizo kabisa, na hapo akipata ukaribu na Mwenyezi Mungu. Matatizo kwa hiyo ni nyenzo yenye nguvu ya kusafisha moyo wa binadamu, na kuiachia ile nafsi ya ndani ing’are. Imam Ali (s) anasema: “Msihofie umasikini na mitihani (majaribu), kwani kwa hakika dhahabu inajaribiwa kwa moto na muumini anajaribiwa kupitia mitihani.”

Mara tu ile haja inapokidhiwa hata hivyo, lile pazia linashuka tena. Yeye sasa anajihisi kutokuwa mhitaji tena na anakuwa mwenye kiburi. Inakuwa kana kwamba hakumhitajia Mwenyezi Mungu kamwe. Mwenyezi Mungu anasema kuhusu mtu kama huyo: Si hivyo! Hakika mtu bila ya shaka hupituka mipaka. Kwa kujiona amejitosheleza. (Q 96-7). Hali hii ya usahaulifu na kutojali inajulikana kama Ghaflat – mughafala, na ni hali ya hatari ya kiakili ambayo inamzuia mtu kulenga na kumzingatia Mwenyezi Mungu na Akhera. Waumini kwa hiyo wanatahadhari juu ya starehe na raha kwani athari ya hali zao za kiroho mara nyingi zinakuwa ni hasi. Imam Musa al-Kaadhim (a) anasema: ‘Hamtakuwa waumini mpaka mchukulie matatizo kama ni neema na starehe kama ni mateso au huzuni, kwa sababu subira wakati wa matatizo ni kubwa zaidi kuliko hali ya kutojali wakati wa faraja.

Vyanzo: Āyatullāh Makārim Shirāzī, al-Amthāl fī Tafsīr Kitaballāh.
Aghā Muhsin Qarā’atī Kashānī, Tafsīr Nūr

Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo