Tafakuri ya 15, Āyat 41: 30 -32; Imani na Umadhubuti

﴾إِنَّ الَّذِينَ قَالُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ثُمَّ اسْتَقَامُوا تَتَنَزَّلُ عَلَيْهِمُ الْمَلَائِكَةُ أَلَّا تَخَافُوا وَلَا تَحْزَنُوا وَأَبْشِرُوا بِالْجَنَّةِ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ ﴿٣٠﴾نَحْنُ أَوْلِيَاؤُكُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَفِي الْآخِرَةِ ۖ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَشْتَهِي أَنفُسُكُمْ وَلَكُمْ فِيهَا مَا تَدَّعُونَ ﴿٣١﴾ نُزُلًا مِّنْ غَفُورٍ رَّحِيمٍ ﴿٣٢﴾
Hakika wale ambao wanasema: Mola Wetu ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakawa na msimamo, huwateremkia Malaika (kuwaambia): Msiwe na hofu, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliokuwa mkiahidiwa. Sisi ni mawalii wenu katika maisha ya dunia na katika Akhera, na humo mtapata kinachotamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata mnavyovitaka. Ni takrima itokayo kwa Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu.
(Sūratu Fussilat, Na. 41, Aaya 30-32).

 

Aya hizi zinaelezea sifa mbili muhimu za muumini:

  • Imani juu ya Mwenyezi Mungu kwamba Ndiye Mola Wao.
  • Umadhubuti (kuwa na msimamo) katika njia Yake

Kuikiri imani ni hatua ya mwanzo tu. Sharti la juu kabisa ni vitendo. Na hatua ya juu zaidi ni ile hali ya Istiqaamah: yaani uimara katika vitendo, kuendelea na kuwa na uvumilivu katika wema. Hicho ndio kipimo cha kweli cha muumini. Waumini wengi wana imani na wanatenda matendo mema. Lakini wanapokabiliwa na dhiki na matatizo, inakuwa vigumu kwao kubakia imara katika imani. Unyonge, uchovu, kushuku mambo kunajipenyeza.

Waumini ambao wana nguvu na dhamira ya kuvumilia baada ya utangazaji wa imani wanatukuzwa kuwa kushuka malaika juu yao ambao wanawanong’oneza ahadi ya malipo ya thawabu nyingi

Wanaahidiwa kwamba:
a) Hawatakuwa na hofu wala huzuni juu yao. Aya nyingi za Qurani zinaahidi uondolewaji wa hofu na huzuni kutoka kwa waumini. Wafasiri wanaeleza kwamba hofu ni kwa ajili ya mustakabali wa matukio ambayo hayajatokea bado. Huzuni ni kuhusu yaliyopita, juu ya dhambi zilizokwisha kutendewa, makosa yaliyofanywa, au matukio yasiyopendeza ambayo yametokea siku za nyuma.
b) Malaika watakuwa walezi na marafiki zao katika dunia hii na kadhalika katika Akhera. Ingawa malaika hawa hawawezi kuonekana au kusikiwa, ulinzi wao na ulezi wao unapitishwa kwa wanadamu kupitia msukumo wa akili. Msukumo huu huleta nguvu na utulivu (sukuun) au amani kwa waumini. Mfano wa nguvu hii isiyoelezeka unaweza  kuonekana katika historia, ambapo makundi madogo ya waumini yaliweza kukabiliana na makundi tofauti makubwa kwa ujasiri na utulivu mkubwa.
c) Malipo ya Pepo yatakuwa yao. Watapewa yote wanayoyatamani, na kuviitisha humo. Heshima kubwa kabisa na starehe kwa ajili ya waumini ni kwamba watapokea malipo yote haya kama wageni wa heshima wa Mwenyezi Mungu ndani ya Pepo. Ingawa kutakuwa na malipo mengi ya kimaada na kimwili ndani ya Pepo, malipo makubwa ya hali ya juu kabisa ni furaha ya kiakili na kiroho inayotokana na kutambua kwamba Mwenyezi Mungu amewaridhia.

Aya hizo hapo juu zinasisitizia umuhimu wa umadhubuti. Umadhubuti au Istiqaamah ni uwezo wa kubakia imara  juu ya kile anachokiamini mtu, na asiwe mwenye kuyumbishwa matamanio, athari za nje, mazingira na hali ya mambo na kadhalika. Hadithi kutoka kwa Imam Ali (a) inasema: Mwenyezi Mungu hapendi viumbe Wake wawe wa rangi nyingi, hivyo msiyumbe na kutoka kwenye ukweli.

Istiqamah yako ina nguvu kiasi gani? Jitahini mwenyewe katika hali hizo hapo juu na uone kama wewe ni mmojawapo miongoni mwa wale ambao malaika watawatembelea na kuwanong’oneza ahadi hizo. Ni uhusiano wa kidunia nyingine uliohifadhiwa kwa ajili ya wale ambao wana nguvu katika imani zao na wamedhamiria kuziendeleza.

Vyanzo: Ayatullah Nasir Makarim Shirazi (mhariri), al-Amthaal fi Tafsiir Kitabillah; Muhammad al-Ray Shahree, Mizanul Hikmah