Tafakuri ya 10, Āyat 28:83: Tamaa ya Ubora

تِلْكَالدَّارُالْآخِرَةُنَجْعَلُهَالِلَّذِينَلَايُرِيدُونَعُلُوًّافِيالْأَرْضِوَلَافَسَادًاۚوَالْعَاقِبَةُلِلْمُتَّقِينَ
Hayo ndiyo makazi ya Akhera, tumewafanyia wale wasiotaka kujitukuza duniani wala ufisadi. Na mwisho ni wa wenye takua.
(Suratul Qasas, Na. 28, Aaya 83)

Aya hii ya Qur’ani Tukufu inayochochea mawazo inashikilia siri ya ukweli mkubwa. Furaha na utukufu katika Akhera vimehifadhiwa kwa ajili ya wale ambao hawana tamaa ya kujikweza juu ya ardhi. Muumini wa kweli huwa hapendelei kuonekana kana kwamba ni bora zaidi ya wengine, au kusifiwa na kutambuliwa katika dunia. Hadithi moja ya Imam Ja’far as-Sadiq (a) inasema:

“Kama ikiwezekana kwa ajili yako, kuwa usiyejulikana. Kwani itakuwaje watu wasipokusifia! Kwani kuna ubaya gani kama kama ukiwa duni mbele ya macho ya watu, wakati ukiwa ni mwenye kustahili sifa mbele ya macho ya Mwenyezi Mungu?”

Wanadamu mara nyingi wana tamaa ya kijiona ni bora kuliko wengine. Tamaa hii ya ubora inachomoza kutoka kwenye ‘Nafsul Ammarah’ ambayo wakati wote inaongozea kwenye maovu, na inaweza kushajiishwa na minong’ono ya Shetani ambaye yeye mwenyewe ana hatia ya ubora wa bandia. Tamaa ya ubora inaweza kuwa kwenye mwelekeo wowote; umaarufu, utajiri, kumiliki mali, elimu, uzuri, kupendwa na watu na kadhalika. Inaweza kutofautiana kuanzia kwenye kutaka kuwa na gari nzuri zaidi kuliko wengine, kutamani kuwashinda wengine katika mabishano au hoja. Katika muundo wowote, mkubwa au mdogo, unalaaniwa sana katika Uislamu. Imaa Ali (a) anasema kwamba hata kama mtu anafurahia kwamba ugwe wa kiatu chake ni bora kuliko ule wa mwenzie, huyo anaweza akaingia chini ya aya  hiyo hapo juu.

Hatati kubwa kabisa ya tamaa hii ya ubora ni kwamba mara nyingi huwa haionekani na haitambuliki. Inajificha chini ya hila za mapato, mafanikio na maendeleo. Nyuma ya sura ya kinafiki ya kutaka kufanya vizuri katika dunia, mwanadamu anakuwa katika kutafuta kuthibitisha kwamba yeye ndiye bora kuliko wengine wote.  Kutafuta huku kunaweza kumpa mafanikio ya mpito katika dunia hii, lakini anaharibu fursa zake za kupata furaha ya milele. Uislamu unahimiza moyo wa matumizi ya vipaji vinavyojaaliwa na Mwenyezi Mungu na njia za kufanikiwa na kuendelea, lakini unashutumu ile nia ya kufedhehesha ya kutaka kuwashinda wengine.

Zifuatazo ni baadhi ya dalili za ugonjwa hatari wa kujitukuza mwenyewe:

1. Kutoridhishwa na maendeleo ya wengine na mafanikio yao katika sifa yoyote ile kutoka kwa wengine na kutaka kuongeleshwa kwa heshima nyingi.
2. Kutumia fursa za kupamba na kuonyesha ustahilifu wake mtu.

Imesimuliwa kwamba wakati wa kipindi cha uongozi wa kisiasa wa Imam Ali (a), yeye Imam wakati mwingi alikuwa akienda sokoni kuwasaidia wengine. Mbali na kuwaongoza wale waliopotea na kuwasaidia wanyonge, Imam alikuwa pia akitumia fursa hizo kutoa ushauri na kuonya. Aliwaendea wafanyi biashara na wachuuzi na kuwasomea aya hiyo hapo juu. Kule kufikiria juu ya aya hiyo kulishusha hisia za ubora wa matajiri juu ya masikini. Imam mwenyewe binafsi alikuwa ni mfano bora wa matumizi ya aya hiyo. Nafasi yake ya Uimam na Khalifa haikumzuia yeye kwenda sokoni na kuwasaidia wale wenye haja.

Imam Ja’far as-Sadiq (a) alikuwa akilia machozi wakati akiisoma aya hii na kusema: “Wallahi, mategemeo yangu yote juu ya dunia hii yametoweshwa na aya hii.” Hii ni kueleza kwamba matumaini yoyote ambayo mtu anaweza akawa nayo katika dunia hii, ya kupata na kulimbikiza, ili kuwa na namna fulani ya ubora juu ya wengine yanapingana na aya hii. Pepo huko Akhera imetengwa tu kwa ajili ya wale ambao hawana haja ya kujikweza na kujitukuzisha katika dunia hii.

Vyanzo: Ayatullah Naasir Makaarim Shiraazii, Al-Amthal fi Tafsiir Kitabillah; Aghaa Muhsin Qara’ati Kashani, Tafsiir Nuur.

Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo