يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ . . . وَتَعَاوَنُواْ عَلَى الْبَرِّ وَالتَّقْوَى وَلاَ تَعَاوَنُواْ عَلَى الإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ وَاتَّقُواْ اللَّهَ إِنَّ اللَّهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ
Enyi mlioamini! . . . Na saidianeni katika wema na takua wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
(Sūratul Maa’idah, Na. 5, Aaya 2).
Katika siku za ujahilia (yaani, zama za kabla ya Uislamu huko Arabuni), watu walikimbilia na kuwasaidia na kushirikiana na wale ambao walitokana miongoni mwa marafiki zao wa karibu na wale wa familia zao, bila ya kuanisha kanuni iliyokuwa nyuma ya kitendo hicho. Ikiwa mtu kutoka kwenye kabila fulani alimshambulia mtu, basi kabila lote litakuwa nyuma yake, hata kama kitendo hicho hakikuwa na haki kabisa. Ushirikiano wa upendeleo kama huo unaweza kuonekana katika ulimwengu wa kisasa pia, ambako nchi zitaunga mkono kwa moyo mmoja kitendo cha washirika wao, hata kama washirika wao hao watakiuka sheria za kimataifa na kuvunja maadili ya kibinadamu.
Aya hii inasisitiza umuhimu wa kushirikiana na kusaidiana katika wema na uchamungu. Ayatullah Naasir Makaarim Shirazi anaelezea katika Al-Amthal fi Tafsir Kitabillah kwamba matumizi ya maneno haya mawili Birr na Taqwa yanavutia sana. Birr au wema ni vitendo vizuri vya uhakika, na Taqwa inazungumzia kukaa mbali na vitendo viovu. Hivyo aya hii inasisitizia ushirikiano wa jambo aina ya chanya – katika kufanya wema na kujiepusha na maovu, na kisha inakataza ushirikiano wa aina hasi – katika vitendo viovu na uchokozi.
Kwa jamii kuendelea katika njia ya kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, ni lazima ifanye kazi kwa pamoja, na kusaidiana kila mmoja wao katika safari hiyo. Kushirikiana na wengine katika wema ni moja kati ya kanuni za msingi kwenye jamii ya Kiislamu. Uislamu unawahimiza wafuasi wake kufanya kazi kwa pamoja kwa wema wa kawaida, na kujiepusha na kufanya kazi kwa pamoja katika mambo ambayo hayafai na machafu. Wakati waumini wanapofanya kazi pamoja kunakuwa na uhamasikaji, shauku na muamko wa moyo. Sambamba na hilo, kunakuwepo na msaada wa kimungu na baraka katika kitendo hicho. Kila muumini anajihisi kutiwa moyo na uwajibikaji wa mwingine, na kwa namna hii, cheche ya wema inaweza kuwa mwanga mkubwa. Kisha mwanga huo huuzingira jamii, miale yake ikiangaza kwenye mambo mbalimbali ya maisha ya wanajumuiya. Kinachoweza kufanikishwa kupitia umoja vitendo kama huo hakiwezi kufanikishwa na mtu mmoja peke yake.
Ushirikiano ni lazima uwe ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu. Mara nyingi watu wanakuwa wanaishiwa hamu na wengine na wanakuwa wasiotaka kufanya kazi pamoja na kusaidiana. Wanahisi kwamba hao wengine hawastahiki msaada wao, na hauwastahili. Hata hivyo, unapofanya kazi nzuri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, unahamasika wakati wote. Mwenyezi Mungu anastahiki lile bora tunaloweza kulifanya, wakati wote. Ukweli wa nia ni muhimu katika ushirikiano wa watu katika jamii ya Kiislamu.
Kushirikiana katika vitendo vizuri kutaongeza wema na uadilifu katika jamii. Njia pekee ya kuzuia kuenea kwa uovu katika jamii ni pale watu wanapokuwa hawafanyi kazi kwa pamoja kwa ajili ya uovu huo – wanapokuwa hawauungi mkono, wanapokataa kusaidiana katika huo na kupitia huo wanaonyesha kutoridhia kwao kitendo hicho. Hili badala yake litapunguza ukuaji wa maovu kama hayo katika jamii.
Chanzo: Āyatullāh Makārim Shirāzī, al-Amthāl fī Tafsīr Kitaballāh.
Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo