إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمْ عَدُوٌّ فَاتَّخِذُوهُ عَدُوًّا
Hakika Sheitani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui
(Suratul Fatir, Na. 35, Aaya 6)
Kumtambua adui maana yake ni kuwa na tahadhari. Hakuna muda wa kuridhika na kutulia hususan pale adui anapokuwa amefichikana, wakati anapoweza kuingia kwenye akili na mawazo yako, na kunong’ona kwenye masikio yako. Adui kama huyo, ambaye anaweza kujipenyeza kwa binadamu anatakiwa kufukuzwa kwa nguvu zote kiasi iwezekanavyo. Maadui wakubwa kabisa wa mwanadamu ni nafsi yake, ile ‘Nafs lawwaamah,’ nafsi ambayo inalingania kwenye maovu, na Shaitan ambaye ameapa kuwapotosha wanadamu wengi tu kwa kadri atakavyoweza. Ni Shaitan huyo huy anayepandikiza mawazo ya uasi na madhambi katika akili na mawazo yetu, ndiye anayechochea ghasia na vurugu, na kuwasha na kuchochea miale ya moto wa migogoro miongoni mwa watu. Ni Shaitan huyohuyo anayecheka sana wakati sisi tunapojisalimisha kwenye mipango na mikakati yake, naye hulia sana pale tunapojilinda na kukataa kuvutwa kuelekea upande wake.
Tunaweza kuwa na hatari dhidi ya Sheitani kama tutaweka chini na kuutelekeza ulinzi wetu. Kama tukiwa macho na kutambua kwamba Shaitan ni adui ambaye wakati wote yupo, basi tutaikataa minong’ono yake. Kila wazo ambalo ni kinyume, kila hisia ambayo ni mbaya na haifai, vyote hivyo lazima vikataliwe kwa nguvu zote. Panda ua/wigo madhubuti kuzunguka bustani ya akili yako na ukatae kabisa kumruhusu kuingia ndani. Yeye hana mamlaka yoyote juu yako isipokuwa yale unayokubali kumpa wewe mwenyewe.
Katika Nahjul-Balaghah, Imam Ali (a) anatuonya kwa ufasaha kabisa kuhusu mitego ya Shetani, anasema: Kwa hiyo unapaswa kuhofia ili yule adui wa Mwenyezi Mungu (Shetani) asije akakuambukiza na magonjwa yake, au asije akakupotosha kupitia sauti yake, auawakusanyie jeshi la wapanda farasi na watembea kwa miguu; (Q 17:64) kwa sababu, naapa kwa uhai wangu, yeye ameweka mshale uangamizao kwenye upinde wake kwa ajili yenu, ameuvuta upinde huo kwa nguvu kabisa na kuwalenga ninyi kutoka mahali pa karibu kabisa…..ikaja kuwa mwenye madhara zaidi katika dini yenu na mchocheaji mkubwa wa miale ya moto wa fitna kuhusu mambo yenu ya kidunia kuliko wale maadui ambao mlionyesha upinzani wa wazi dhahiri na ambao dhidi yao mlikusanya majeshi yenu. Kwa hiyo mnapaswa kutumia nguvu zenu zote dhidi yake, na pia juhudi zenu zote dhidi yake. (Nahjul-Balaghah, Hotuba ya 192).
Isome aya hii kila wakati sauti yako ya ndani inapoanzisha mazungumzo hasi na kinyume pamoja na wewe. Itambue minong’ono ya Shetani kwa namna vile ilivyo hasa – mishale inayorushwa na adui kukulenga wewe. Irushe kumrudishia mwenyewe na uthibitishe nguvu na umahiri wako. Jivishe vazi la imani na ubebe ngao ya taqwa. Unaweza kushinda vita hivi na ukawa miongoni mwa wale ambao Shetani amekata tamaa juu yao.
Vyanzo: Amirul-Mu’miniin Ali (a); Nahjul-Balaghah; Ayatullah Makaarim Shiraazii (ed), al-Amthal fi Tafsiir Kitabillah