قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ * الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ
Hakika wamefaulu waumini. Ambao ni wanyenyekevu katika Swala zao.
(Surah Al-Mu’minun, Na. 23, Ayah 1-2)
Kila mmoja anapenda kufanikiwa. Lakini ni yapi mafanikio ya kweli? Kigezo cha mafanikio kinaweza kikatofautika kutoka mtu mmoja hadi mwingine; hivyo tunahitaji kile kigezo kutoka kwa Muumba, ambaye anajua kwa hakika kwamba mafanikio ni nini hasa. Mafanikio yameelezwa kama ni mtu kutimiza mahitaji yake na kupata furaha, kuvishinda vikwazo katika kutafuta kupanda juu.
Chochote kinacholeta mafanikio katika ulimwengu huu ni chenye uhai mfupi na cha mpito. Ni chenye uwezekano wa kupatwa na madiliko. Maisha katika dunia hii yana magumu na mepesi yake, na hakuna mwenye mafanikio ya kudumu. Hivyo ni furaha ya mpito ambayo haiwezi kutegemewa. Mafanikio katika Akhera hayaguswi na utamaduni wa mpito kama huo. Wale watakaopata furaha huko watakuwa na uwezo wa kuidumisha furaha hiyo milele. Hivyo mafanikio ya kweli ni yale ambayo yatapatikana katika ulimwengu ule ujao.
Mwenyezi Mungu katika kifungu hiki cha maneno anaelezea sifa za waumini wenye kufaulu hasa. Sifa yao ya kwanza ni kwamba ni wanyenyekevu wanapozungumza na Mwenyezi Mungu. Unyenyekevu ni hali ya ndani kabisa ya uungwana unapokuwa mbele ya nafsi mashuhuri na yenye mamlaka makubwa. Hali hii ya ndani kabisa huwa inadhihirika katika vitendo na miondoko ya mwili. Unyenyekevu katika swala ni dalili ya moyo wenye afya njema, ule ambao haukudumazwa na maradhi ya kiburi na majivuno.
Unyenyekevu hasahasa ni kitu gani? Imam Ali (a) wakati mmoja aliulizwa kuhusu unyenyekevu naye akasema: “Ni kuwa dhalili kakika Swala na kugeukia kwa Mwenyezi Mungu kwa moyo wote (Mustadrakul-Wasa’il, Jz. 1, uk. 98). Amesema vilevile kwamba: “Mwenyezi Mungu anao waja wake ambao nyoyo zao zimejawa na unyenyekevu, hivyo wanajizuia na mazungumzo marefu (maneno mengi) ingawa ni wafasaha wa maongezi, wenye akili sana. (Biharul-Anwaar, 66:284). Unyenyekevu ni utambuzi makini wa udhalili wa mtu mwenyewe na Utukufu wa Mwenyezi Mungu swt. Ina maana ya kuwa na utambuzi wa dhambi zote zilizotendwa.
Inajumuisha kuzidiwa wakati mwingine na mawazo ya mja wa Mungu asiyemiliki chochote, aliyesimama kwenye mlango wa Yule ambaye ni Bwana (Mola) wa kila kitu, na kuruhusiwa kuingia na kuwa na mazungumzo binafsi pamoja Naye. Unyenyekevu ni ufunguo wa kuiswali swala vile inavyotakikana kuswaliwa. Mtu mwenye unyenyekevu (khushui) huswali kwa namna ya utulivu na utaratibu, polepole. Ni mtulivu katika swala, mwenye kujihisi kuwa na haya, na bado ni mwingi wa matumaini na mapenzi juu ya Mwenyezi Mungu. Soma aya hii ili kujikumbusha mwenyewe juu ya unyenyekevu na udhalili unaotakikana katika swala. Kutengeneza njia yako kuelekea kwenye ufaulu, hiyo ndio sifa ya kwanza ambayo ni lazima uipate.
Chanzo: Ayatullah Makaarim Shiraazii (mh); al-Amthal fi Tafsiir Kitabillah
Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo