ثُمَّ قَسَتْ قُلُوبُكُم مِّن بَعْدِ ذَٰلِكَ فَهِيَ كَالْحِجَارَةِ أَوْ أَشَدُّ قَسْوَةً ۚ وَإِنَّ مِنَ الْحِجَارَةِ لَمَا يَتَفَجَّرُ مِنْهُ الْأَنْهَارُ ۚ وَإِنَّ مِنْهَا لَمَا يَشَّقَّقُ فَيَخْرُجُ مِنْهُ الْمَاءُ ۚ وَإِنَّ مِنْهَا لَمَا يَهْبِطُ مِنْ خَشْيَةِ اللَّـهِ ۗ وَمَا اللَّـهُ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ
Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu bada ya hayo, zikawa kama mawe au ngumu zaidi; kwani katika mawe kuna yanayobubujika mito ndani yake, na katika hayo kuna yanayopasuka yakatoka humo maji; na katika hayo kuna yanayoanguka kwa sababu ya kumwogopa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu si Mwenye kughafilika na mnayoyafanya. (Suratul Baqarah 2: Ayah namba 74)
Aya hiyo hapo juu inawarejelea Wana wa Israeli ambao waliambiwa watoe kafara ya ng’ombe na kumpiga mtu aliyeuawa kwa sehemu ya ng’ombe huyo. Halafu mtu huyo atakuwa hai na atawaeleza muuaji wake alikuwa ni nani.
Visingizio vingi na maswali mengi wana wa Israili waliyomuuliza Nabii Musa (a) kuhusu hili, na kusita kwao kwa dhahiri kufanya kama walivyoamrishwa yote hayo yanashutumiwa na Mwenyezi Mungu katika aya hii. Tabia yao hiyo iliishia kwenye kuwa na ugumu wa mioyo. Moja ya maradhi yanayousibu moyo ni ugumu (ususuavu) wa moyo unaojulikana kwa Kiarabu kama Qaswatul-Quluub.
Ayatullah Dastghayb katika kitabu chake, Qalbi Saliim, anaelezea Qaswat kama ugonjwa wa kiroho unaomzuia mwanadamu kukubali ukweli, na kunyenyekea au kuwa na hofu juu ya Mamlaka Ya Juu. Ugumu wa moyo ni maneno ya kiistiari yenye maana ya hiari kwenye ushauri na maonyo. Moyo unakuwa hauathiriki na mandhari au matukio ambayo yanaamsha hisia kama vile malalamiko ya wanaodhulumiwa na vilio vya mayatima. Kwa jumla unakuwa baridi na mgumu kama jiwe.
Katika aya hiyo hapo juu, moyo wa mwanadamu ambao ni mgumu unatangazwa na Mwenyezi Mungu kwamba ni mgumu zaidi kuliko hata mawe. Sababu tatu zinatolewa kwa ajili ya hili:
1) Mawe (majabali) mengi yana mito na mifereji ya maji inayotiririka kutoka humo. Lakini hakuna chochote kinachotoka kutoka kwenye moyo mgumu. Unakuwa hauna hisi zote za kibinadamu.
2) Mawe wakati mwingine hupasuka na kuvunjika vipande vipande kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Mvua na upepo huathiri maumbile ya mawe na kusababisha mabadiliko katika sura na muonekano. Lakini moyo mgumu hauathiriwi na chochote. Hakuna ulinganio, ushauri na maonyo yanayoweza kusababisha mabadiliko yoyote ndani ya moyo huo.
3) Majabali mengine huanguka chini mbele ya mamlaka na uwezo wa Mwenyezi Mungu. Magumu kama yalivyo, utukufu wa Mwenyezi Mungu bado ni mkubwa na unayashinda. Lakini moyo mgumu hausalimu amri kwenye nguvu ya Mwenyezi Mungu. Matendo yote ya mwanadamu yanachipukia kutoka moyoni, na moyo mgumu huwa hauzalishi matendo yoyote mema. Hadithi nyingi zinasisitizia kuhusu umuhimu wa kuutibia moyo kutokana na ugumu ili kupata mafanikio ya kweli.
Mtukufu Mtume (s) anasema: “Mtu aliyeko mbali sana na Mwenyezi Mungu ni yule mwenye moyo mgumu.” Imam Ali (s) anasema: “Bahati mbaya kubwa kabisa ni kuwa na ugumu wa moyo.” Moyo wa binadamu haukuumbwa mgumu. Moyo wa mtoto mdogo ni laini sana na wenye huruma na upendo. Mtu mzima hata hivyo, kupitia ulimbikizaji wa dhambi na tabia ya kutojali, kidogo kidogo hupatwa na moyo mgumu. Ukiachwa bila kutibiwa, unaweza kuwa kama ulivyoelezwa hapo juu, kuwa mgumu zaidi hata kuliko mawe. Ni wajibu wa kila Muumini kuwa mwangalifu juu ya hali ya moyo wake na kuchukua hatua za kuuepusha kuwa mgumu.
Chanzo: Ayatullah Makaarim Shiraazii (mhariri); al-Amthal fi Tafsiir Kitabillah
Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo