Tafakuri ya 18, Āyāt 14: 24 – 25; Neno Zuri

كَلِمَةً طَيِّبَةً كَشَجَرَةٍ طَيِّبَةٍ أَصْلُهَا ثَابِتٌ وَفَرْعُهَا فِي السَّمَاءِ ﴿٢٤﴾ تُؤْتِي أُكُلَهَا كُلَّ حِينٍ بِإِذْنِ رَبِّهَا
Neno zuri; kama mti mzuri, mizizi yake ni imara na matawi yake yako mbinguni. Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola Wak
(Surat Ibrahim, Na 14, Ayat 24-25).

 

Lile neno zuri katika mti huu limeelezewa kama ni yale maneno na matendo ya mwanadamu ambayo yanachipukia kutoka kwenye imani na Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anayalinganisha na mti ambao una nguvu, uliosimama wima na wenye kuzaa vizuri – sifa ambazo zinamstahiki mu’mini. Maneno na vitendo vya mu’mini yanapendeza kama mti mzuri.

Kuyalinganisha na mti mzuri kunaelekeza kwenye yafuatayo:
– Neno zuri lina makuzi na maendeleo. Halikwami na kudorora. Lile ambalo linafanywa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu wakati wote huwa linakua.
– Kila sehemu ya hilo neno zuri ndio ubora wake unaowezekana. Mzizi wake ni imara, matawi yake yako juu kabisa, na matunda yanazaliwa kila msimu. Huyo ndio mu’mini. Mtukufu Mtume (s) alisema: “Mu’umini ni sawa na mti wa mtende, kila sehemu yake ina manufaa.”
– Kuwa na mizizi madhubuti kunauwezesha mti kuwa na matawi ya juu, na matunda ya wakati wote. Bila ya kuwa na mizizi madhubuti hilo lizingewezekana. Kadhalika, kila kinachofanywa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu lazima kiwe kimesimikwa katika imani thabiti, kwa ajili ya chenyewe kuweza kufikia juu.
– Matawi ya mti huo yako juu zaidi ya usawa wa ardhi, mbali kabisa na uduni na uchafu wa ardhi. Kadhalika, maneno na vitendo vya muumini viko juu kabisa ya viwango visivyo na muhimu vya matamanio ya kidunia.

Kuzungumza maneno mazuri yenye kuvutia ni dalili ya imani. Mtukufu Mtume (s) amesema: “Yeyote  anayemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Kiyama basi naaseme maneno mazuri ama anyamaze kimya.” (Nahjul Fasaha Hadithi ya 2915). Ni haki ya ulimi kwamba unapaswa kutumika kwa wema tu. Imam Zaynul Abidiin (a) analielezea hili katika Risalatul Huquq hivi: “Ni haki ya ulimi kwamba ni lazima uuchukulie kwamba ni wenye kuheshimika kiasi cha kutoweza kutamka lugha chafu; na ni lazima uuzoeshe kwenye mazungumzo mazuri na uunadhimu na tabia njema, na uuweke kimya isipokuwa katika nyakati za lazima na muhimu, na kwa ajili ya manufaa ya kiroho  na kimaada, na uuweke mbali na mazungumzo yasiyo na maana ambayo yanaweza kusababisha madhara makubwa mno na faidi kidogo kabisa, na uwe mpole kwa watu na useme yaliyo mazuri kuwahusu wao.

Hii ni aya nzuri sana ya kukukumbusha wewe mwenyewe kuongea maneno mazuri. Jihamasishe wewemwenyewe kusema maneno ambayo ni kama miti – yenye nguvu, bora kabisa na yenye kuzaa matunda. Matunda ya maneno yako yanaweza kubakia katika akili na nyoyo za watu kwa muda mrefu kuliko unavyotegemea.

Vyanzo: Āytaullāh Nāsir Makārim Shirāzī (mhariri), Tafsīr-e Namūneh;
Imam Zaynul Abidin (a), Risalatul Huquq

 

Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo