Tafakuri ya 17, Āyat 37:99 SAFARI KUELEKEA KWA MOLA

وَقَالَإِنِّيذَاهِبٌإِلَىٰرَبِّيسَيَهْدِينِ

Na akasema: Hakika mimi nahama, nakwenda kwa Mola wangu Mlezi;
Yeye ataniongoa
(Suratus Sāffāt, Na. 37, Āyat 99)

 

Aya hii ni kauli ya Nabii Ibrahim (a) baada ya kutoka kwenye ule moto, salama na bila kudhurika. Anaondoka kuhamia sehemu nyingine, na anawaambia watu kwamba ninaondoka kuelekea kwa Mola Wangu ambaye ataniongoza mimi.
Ina maana gani huku kwenda kwa Mola Wako, wakati Mwenyezi Mungu hana mahali? Jibu linapatikana katika kuelewa kwamba kuelekea kwa Mwenyezi Mungu ni safari ya kiroh. Ina maana kwamba:

  • Kuondokasehemu chafu iliyonajisika na kwenda kwenye tohara
  • Kwenda kwenye sehemu ambako umaweza kuwa peke yako na Mwenyezi Mungu tu.
  • Kutafuta mahali mbali na watu ili kumuomba Mwenyezi Mungu haja zake mtu (Hicho ndicbo Nabii Ibrahim (a) anachokifanya katika aya ifuatayo).
  • Kujiweka mbali kihisia kutokana na yale yote mbali na  Mwenyezi Mungu.
  • Kujielekeza mwenyewe kwa Mwenyezi Mungu kwa akili yako (nia), mwili (matendo) na moyo (hisia),

 

Nabii Ibrahim (a) alinuia kuondoka Babeli kuelekea Syria ambako angeeneza neno la Mungu. Kusafiri kwake kulikuwa ni kwenda mahali ambapo atapokea ujumbe wa Mwenyezi Mungu na kuufikisha kwa wengine. Alikuwa anahama ili aweze kutimiza majukumu yake ya Utume. Kiongozi wake katika safari hii atakuwa ni Mwenyezi Mungu. Tafsiir Nuur inasema kwamba Imam Ali (a) aliielezea safari akisema kwamba kuelekea kwa Mwenyezi Mungu ni mtu kutoa mazingatio kwa Mwenyezi Mungu na kumfanya Yeye kuwa ndio shabaha ya maisha. Wale ambao wanampenda Mwenyezi Mungu kamwe hawatajihisi kuwa mtegoni. Wakati wote watapata njia ya kuwapeleka kwa Mwenyezi Mungu.
Sisi sote ni wasafiri kuelekea kwa Mwenyezi Mungu. Maisha ni safari, na kila pumzi ya uhai tunayovuta inatupeleka hatua moja zaidi, karibu na mafikio ya mwisho, ambako tutajumuika na Muumba ambaye alitutuma sisi kwenye dunia hii. Inaweza ikawa ni safari ya marejeo ya kupendeza, kuungana tena na Mpendwa, iwapotu tutaiandaa kwa uangalifu. Safari hiyo inaweza ikawa ni safari ya nje, wakati muumini anahama kwa sababu haoni mahali pake pa sasa kwamba panaendana na ukuaji wa kiroho. Lakini safari ya ndani pia ni muhimu. Muumini lazima ahame kutoka kwenye uovu kwenda kwenye wema, kutoka kwenye ushirikina kwenda kwenye tawhiid, na kutoka kwenye dhambi kwenda kwenye utiifu. Wakati muumini anapochukua safari kama hiyo kiongozi wake katika safari yote hiyo ni Mwenyezi Mungu.
Soma aya hii ili kujikumbusha mwenyewe kwamba uko safarini kuelekea kwa Mwenyezi Mungu. Unayo njia ya kutembea juu yake, na kama wengine hawataki kufuatana na wewe, bado itakubidi kuendelea kusafiri. Kama utatembea juu ya njia ielekeayo kwa Mwenyezi, Yeye atakuongoza na kuifanya nji hiyo kuwa nyepesi kwa ajili  yako.

VYANZO: Āytaullāh Nāsir Makārim Shirāzī (ed), Al-Amthaal fi Tafsiir Kitabillah; Aghae Muhsin Qaraati, Tafsire an-Nuur

Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo