Tafakuri ya 16, Āyat 90:1 – 4; Hatari za Raha na Starehe

لاَ أُقْسِمُ بِهَذَا الْبَلَدِ* وَأَنْتَ حِلٌّ بِهَذَا الْبَلَدِ* وَوَالِدٍ وَمَا وَلَدَ* لَقَدْ خَلَقْنَا الإِنسَانَ فِي كَبَدٍ
Naapa kwa mji huu! Nawe unaukaa mji huu. Na kwa mzazi na alichokizaa! Hakika tumemuumba mtu kwa tabu
(Suratul Balad, Na. 90, Ayat 1-4).

Katika aya hizo hapo juu, Mwenyezi Mungu anatangaza ukweli muhimu; ukweli ambao unaweza ukawa usio wenye kupendeza kwa mwanadamu. Maisha ya wanadamu mara nyingi ni yenye tabu na dhiki. Mwanadamu angependa maisha yaliyojaa furaha na starehe, lakini hicho sicho alichokipanga Mwenyezi Mungu kwa ajili yake katika dunia hii. Raha na starehe hazipatikani katika kile ambacho Mwenyezi Mungu anakichagua kwa ajili ya mwanadamu. Ile ardhi ambayo Nabii Ibrahim (a) alimuweka mkewe na mtoto wake kulingana na amri ya Mwenyezi Mungu ilikuwa ni ardhi kavu na kame. Qurani inasema: “. . . na wakati Ibrahim aliposema: Ewe Mola Wetu! Hakika mimi nimeweka baadhi ya dhuria zangu katika bonde lisilokuwa na mmea, kwenye nyumba Yako takatifu, ewe Mola Wetu, ili wasimamishe Swala (Q 14:37). Hapa ndipo mahali palipochaguliwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya sehemu takatifu zaidi, mahali pa usalama na ibada.

Binadamu wanapenda starehe na anasa. Lakini starehe nyingi ina madhara. Adha za maisha zinamsaidia mwanadamu kukua na kukomaa. Hicho ndicho Mwenyezi Mungu anachotaka kutoka kwake, kusonga mbele juu ya njia ya kuelekea kwenye ukamilifu. Wakati mwanadamu anapojiendekeza mwenyewe na kujipatia kila aina ya starehe, anakuwa amejielekeza kwenye madhara yafuatayo:
Kiburi: Wakati mwanadamu anapozungukwa na starehe na furaha huwa anaelekea kuasi na kujiona mwenyewe kama si mhitaji. Mwenyezi Mungu anasema: “Si hivyo! Hakika mtu bila ya shaka hupituka mipaka. Kwa kujiona amejitosheleza.” (96:6-7). Vilevile kinamzuia kuhisi huruma juu ya wengine. Hawezi kulihimiza hilo kwani yeye binafsi hajapata kupitiwa na lolote lile bali starehe tu.

Uvivu. Moyo unakuwa wenye kudai na kudai zaidi vile unavyokuwa unapewa anasa. Utakataa kufanya chochote ambacho ni mzigo, au ambacho kinaelekea kuwa kigumu. Unajiepusha na kazi ngumu, iwe ya kimwili au kiakili, na hicho kinakuwa ni kikwazo kwenye maendeleo. Kwa mujibu wa Imam Ali (a): ‘Kikwazo cha kwenye mafanikio ni uvivu.’

Kutokukomaa: Mtu ambaye amezoea starehe na raha nyingi huyo bado hajakabiliana na uhalisia wa dunia. Yeye kwa hiyo mara nyingi anakuwa hajakomaa na kupevuka katika kufikiri kwake, uvumilivu wake na uwezo wa kushughulika na dunia. Kama vile alivyojizoesha kwenye starehe za kimwili, vilevile atatarajia kwamba hisi zake na kufikiri kwake kutakuwa kwa starehe na hakutatibuliwa na watu wengine. Hili litamsababishia kuvunjikiwa na matumaini kwingi sana katika maisha.

Mapenzi makubwa ya Dunia: Raha nyingi katika dunia hii zinasababisha kuipenda zaidi dunia. Inakuwa vigumu kuachana nayo. Kifo kinachukiza kwa sababu ndio mwisho wa aina hizi za starehe na anasa. Wakati Abu Dharr alipoulizwa ni kwa nini watu wanakichukia kifo alisema: “Mmeiimarisha na kuizatiti dunia hii na kuibomoa ya Akhera. Hivyo hamtaki kuhama kutoka kwenye maimarisho na kwenda kwenye uharibivu.”

Isome aya hii ili upate kutambua vyema manufaa ya dhiki na taabu, na kujua nafasi inayochukua katika maisha yetu.

Vyanzo: Ayatullah Nasir Makarim Shirazi (mhariri), al-Amthaal fi Tafsiir Kitabillah; Muhammad al-Ray Shahree, Mizanul Hikmah 

 

 

Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo