وَإِنْ تَعْفُوا وَتَصْفَحُوا وَتَغْفِرُوا فَإِنَّ اللَّهَ غَفُورٌ رَحِيمٌ
Na mkisamehe, na mkapuuza, na mkaghufiria, basi Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu.
(Suratul Taghābun, Na. 64, Ayat 14)
Aya hii inazungumzia kuhusu hatua tofauti za msamaha. Kwa mujibu wa Tafsiir, aya ya 14 ya Surat-Taghbuun ilishuka baada ya wake fulani kujaribu kuwazuia wale Waislamu wa mwanzoni kuhama. Baadhi ya Waislamu waliwasikiliza wake zao, ambapo wengine walikataa na kuwakasirikia. Hii ndio maana sehemu ya kwanza ya aya hii inasema: “Enyi mlioamini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu ni maadui zenu; basi tahadharini nao.” Mwenyezi Mungu anawaambia kwamba familia haipaswi kuwavuguga kutokana na kufanya jambo la sawasawa, lakini ikiwa watabadilika baada ya hilo, basi waumini wanapaswa kuwasamehe.
Kuna hatua tatu za msamaha zilizotajwa katika aya hii. Ili kumsamehe hasa mtu, unahitaji kupitia hatua zote tatu:
Msamaha au kuwia radhi. Hili limeelezewa kama kutotilia maanani kosa lililofanyika. Kwa mujibu wa Imam Ali (a), Msamaha ndio taji la sifa zote za kiungwana. Kusamehe kunaweza kujumuisha na kumuwia radhi mtu huyo, kumpatia nafasi, kuelewa udhaifu wake, kutolichukulia kwa uzito sana na kutolisisitizia kwa mfululizo. Kupita kwenye hatua hii kunaongeza kasi mchakato wa msamaha halisi.
Safh au Uvumilivu: Hii ina maana ya kujizuia kuadhibu,kwa maneno au vitendo. Wakati mwingine tunasamehe, lakini hatuwezi kuizuia ile tamaa ya kuzungumzia kuhusu jambo hilo, na kumkumbusha huyo mtu mwingine juu ya maumivu aliyotutia. Maneno, vitendo vya kihisia na hata hisia zenyewe, hivyo ni ukumbusho endelevu juu ya maudhi ambayo “tumeyasamehe” lakini hayawezi kupita na kuondoka akilini. Usamehevu wakweli unahitajia ustahimilivu. Kama tumekwenda na hatua ya kwanza kwa uangalifu na umakini, hii ya pili itakuwa rahisi. Qur’ani Tukufu inasema: “…..Basi samehe msamaha mzuri.” (Q 15:85). Imam Ali ar-Ridhaa (a) katika kulielezea neno ‘Safh’ katika aya hii anasema inamaanisha: ‘kumuwia radhi na kumsamehe mtu bila ya adhabu, ukali au makemeo.’
Ghufran au Msamaha: Msamaha una maana ya kufuta kile kitendo ambacho kimefanywa na kkuondoa yale matokeo hasi ambayo kitendo hicho kinayasababisha. Wakati Mwenyezi Mungu anasamehe tendo, hatamuadhibu mtendaji kwa ajili ya kutenda hivyo. Linaondolewa kabisa kutoka kwenye kitabu cha matendo. Kumsamehe mtu maana yake ni kwamba hakuna hata fikira ya kulipiza au kuchukua kisasi.
Kusamehe ni tabia moja nzuri sana, lakini ni ngumu kuitimiza…..Hata pale inapokuja, huwa mara nyingi imeambatana na wasiwasi fulani. Watu watasamehe, lakini bado watabaki na mfundo. Hatua za usamehevu zinamsaidia mwenye kusamehe kufikia msamaha wa kweli, bila ya masharti yoyote. Ni katika ubinadamu kule kukumbuka, kwa vile uwezo ama hisi ya kumbukumbu ni sehemu ya binadamu wote, lakini ni vipi tunakumbuka ndio jambo la muhimu. Msamaha wa kweli una maana ya kukoma kwa hisia za hasira na ukinyume kwenye kumbukumbu ya tukio lenyewe.
Soma aya hii ili kujikumbusha mwenyewe juu ya umuhimu wa kusamehe na haja ya kupiti hatua zote hizi za msamaha.
Chanzo: Ayatullah Mohammad Husain Tabatabai, Tafsir al-Mizan
Ayatullah Nasir Makarim Shirazi (mhariri), al-Amthal fi Tafsiir Kitabillah
Agha Muhsin Qara’ati Kashani, Tafsiir an-Nuur
Muhammad al-Ray Shahree, Mizanul Hikmah
Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo