Tafakuri ya 13, Āyat 2:21- Taqwa: Kumtambua Mwenyezi Mungu

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِنْ قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ
Enyi watu! Mwabuduni Mola Wenu ambaye amewaumba ninyi na wale wa kabla yenu,
ili mpate kuwa na takua.

(Sūratul Baqarah, Na. 2, Aya 21)

Aya hii ndio amri ya kwanza ndani ya Qurani Tukufu, inayomwambia binadamu amuabudu Yule Mmoja aliyemuumba yeye na wale wa kabla yake. Amri hii inakuja baada ya vifungu vinavyomuelezea muumini, asiyeamini na munafiki. Yeye swt anaelezea jinsi waumini walivyoongozwa kuelekea kwa Mwenyezi Mungu, na Qurani ndio mwongozo wao. Wale wasioamini wana mifuniko (mihuri) kwenye nyoyo zao kwa matokeo ya vitendo vyao viovu, na wanazembea kuhusu hali zao. Wanafiki ni wale ambao wana maradhi katika nyoyo zao, na vitendo vyao vinaongeza maradhi.

Baada ya kuzungumzia kuhusu sifa za makundi haya matatu, Mwenyezi Mungu sasa anashauri utaratibu rahisi kwa ajili ya mafanikio ya kweli na ukamilifu wa binadamu. Ibada na kumtambua Mwenyezi Mungu ndio jambo moja tu ambalo linamtofautisha muumini na linamnyanyua hadi kwenye hadhi ya Khalifa wa kweli. Ni mwaiko kwenye Tawhiid halisi na ukanaji wa miungu mingine yote.Unaongozea kwenye lengo la mwisho kabisa. Taqwa ama utambuzi wa Mwenyezi Mungu

Ibada imeelezewa na wanachuoni kama ni yenye hatua tatu:

  1. Ibada ambayo ni sahihi. Hii ni wakati muumini anatafuta masharti na hali muhimu kama vile tohara, utaratibu, muda na kadhalika.
  1. Ibada ambayo inakubalika. Hii ni ibada ambayo inafanywa kwa taqwa – utambuzi wa Mwenyezi Mungu, au uchamungu.
  1. Ibada ambayo inaleta ukamilifu. Hii ni ibada ambayo inafanywa kwa sifa za utambuzi, heshima iliyochanganyika na hofu, mapenzi na hali ya faragha.

 

Ibada ya kweli ni ile ambayo inafanywa kwa moyo wa shauku na mapenzi. Mtukufu Mtume (s) anasema: “Mbora wa binadamu ni yule ambaye anaipenda mno ibada na kuifuatilia kivitendo; anaipenda kwa moyo, anaitekeleza kwa mwili wake, na anaitengea muda. Kisha hajishughulishi sana kuhusu dunia, ima iwe ngumu au rahisi.”

Taqwa ndio lengo la ibad. Ibada haiongezi chochote kwa Mwenyezi Mungu, wala kukosekana kwa ibada hiyo hakumpunguzii Yeye chochote. Yeye ni Mola wa utukufu, pamoja na kuwepo au kutokuwepo kwa ibada ya Viumbe. Faida ya Taqwa inarejea kwa binadamu wenyewe. Athari za Taqwa zinamnyanyua katika hadhi, zinampatia sifa za kiungwana na kamilifu na zinamsaidia kutambua uwezo wake na lengo la kuumwa.
Haya ni mafanikio kwa mwanadamu. Qurani inasema katika Suratul Baqarah: Na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu. (Q2:189).

Chanzo: Ayatullah Nasir Makarim Shirazi (mhariri) al-Amthal fi Tafsiir Kitabillah.

Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo