أَنْزَلَمِنَالسَّمَاءِمَاءًفَسَالَتْأَوْدِيَةٌبِقَدَرِهَافَاحْتَمَلَالسَّيْلُزَبَدًارَابِيًاۚوَمِمَّايُوقِدُونَعَلَيْهِفِيالنَّارِابْتِغَاءَحِلْيَةٍأَوْمَتَاعٍزَبَدٌمِثْلُهُۚكَذَٰلِكَيَضْرِ
بُاللَّهُالْحَقَّوَالْبَاطِلَۚفَأَمَّاالزَّبَدُفَيَذْهَبُجُفَاءًۖوَأَمَّامَايَنْفَعُالنَّاسَفَيَمْكُثُفِيالْأَرْضِۚكَذَٰلِكَيَضْرِبُاللَّهُالْأَمْثَالَ
Ameteremsha maji kutoka mbinguni na mabonde yakamiminika maji kwa kadiri yake na mvo ukachukua mapovu yaliyokusanyika juu yake. Na katika vile wanavyoyeyusha katika moto kwa kutaka mapambo au vyombo vingine hutokea povu mfano wake. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopiga mfano wa haki na batili. Ama povu linakwenda bure; ama kinachowafaa watu hukaa kwenye ardhi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopiga mifano.
( Suratul Ra‘d, Na.13, Aya 17).
Aya hii ya Qur’ani yenye kusisimua imejaa maana na kina. Mfano anaoutoa Mwenyezi Munatika aya hii ni ule wa mvua ambayo inanyesha juu ya ardhi. Sehemu mbalimbali za ardhi zinaipokea kulingana na uwezo wao. Kisha maji yanamiminika na povu likitanda juu yake. Povu hili ni sawa na fuo linalotoka wakati chuma kinapoyeyushwa. Mwenyezi Mungu analifananisha povu na fuo kama batili, ambapo yale maji yanayobakia pamoja na yakawa na manufaa kwa watu yanafananishwa na haki.
Kutafakari juu ya aya hii kunafichua maana nyingi zilizofichika. Kupitia mifano hii, Mwenyezi Mungu anatutaka sisi tutambue ile tofauti kati ya haki na batili. Kwa kutumia mfano ambao kila mtu anaweza kuuona, Mwenyezi Mungu anatuonyesha mambo mepesi ambayo mara nyingi huwa hatuyajali au tunayapuuza. Ni wangapi kati yetu wameona povu linalotanda juu ya maji na wakalitoa kama uchafu wa kawaida usio na faida! Kwetu sisi maumbile ni ya kuonekana na kufurahiwa, au pengine kuonekana na kuchukuliwa kama uthibitisho wa kuwepo Muumba. Lakini katika aya hii Mwenyezi Mungu anatutaka tufike mbali zaidi ya hapo. Anatutaka tupate umaizi kutokana na kuchunguza lile povu na fuo linalotengenezwa katika maumbile.
Mwalimu mmoja wa Qurani alieleza kufutiwa kwake na aya hii katika somo akisema kwamba kwa hakika wakati mmoja alitoka nje wakati mvua ikiwa inanyesha, na akaangalia vile mji yanavyodondoka juu ya ardhi, akaifuatilia ile njia ya maji hayo yalivyokuwa yakitiririka, na akaliangalia lile povu wakati lilipoanza kuvimba. Hakuwahi kamwe kulichunguza jambo hili kwa macho ya tafakari kama hayo. Aliliona povu hilo likipanda na kububujika kwenda mbele, lakkini akaliona likitulia wakati maji yalipotiririka kuelekea kwenye maeneo ya ardhi yaliyolala zaidi. Hatimae povu hilo likatoweka na maji nayo yakatulia. Kitu alichogundua ni asili ya kutodumu ya batili.
Wafasiri wa Qurani wametoa mambo mengi wakati wakizungumzia kuhusu aya hii. Baadhi ya mambo yameelezwa kwa mukhtasari hapa chini:
1. Mvua inanyesha kwa kiwango sawa juu ya mgongo wa ardhi, bali upokeaji na unyonyaji wa ardhi unategemea juu ya hali ya udongo. Baadhi ya udongo unaweza kunyonya maji ya kutosha kwa ajili ya uoteshaji, na maji hayo huugeuza kuwa ni mahali penye rutuba. Aina nyingine za udongo zitakuwa hazina uwezo wa kunyonya maji mengi na zitabakia kuwa kame. Namna hiyo ndio mfano wa Wahyi mtukufu na moyo wa mwanadamu.Hekima na muongozo kutoka kwa Mwenyezi Mungu unakuja kwa ajili ya kila mtu, lakini kila binadamu hupokea na kupata manufaa kutokana nao kulingana na uwezo wake.
2. Haki na batili wakati mwingine inakuwa vigumu kuzitofautisha. Mara kwa mara batili huwa imegeuzwa sura na kuwa katika umbile la haki, na ina watetezi wengi mno ambao wataichukulia dhamana. Jambo hili ni kweli hasa katika dunia ya kisasa ya leo hii, ambapo haki na batili katika masuala ya uadilifu na unyofu mara nyingi hayatofautishiki. Katika aya hiyo hapo juu, Mwenyezi Mungu anatupa dalili zifuatazo ili kuweza kutofautisha kati ya haki na batili:
- Haki wakati wote ni yenye manufaa na faida. Kama maji yale yanayotiririka ambayo ni chanzo cha uhai. Haki inakipa uhai na msukumo kila kitu inachokutana nacho. Batili kwa upande mwingine haisaidii kitu na ni yenye kukithiri. Lile povu juu ya maji halizimi kiu yoyote wala kusababisha uoto wowote wa kijani kumea. Halina faida yoyote kwa mwanadamu.
- Batili siku zote inakuwa juu, ikifanya makelele mengi na vitendo vya ghasia. Inavuta nadhari na kuonekana kama kubwa sana, lakini kama povu, inakuwa iko tupu ndani yake. Haki ni nyenyekevu, kimya na iko tayari kuridhika kubakia kuwa chini. Yenyewe ina uzito na thamani, na haihitaji kuvuta nadhari ili kupata kuthaminiwa. Imam Ali (a) anasema: “Haki ni nzito na nzuri, wakati ambapo batili ni nyepesi na iliyochafuka.”
- Haki ina nguvu na wakati wote huwa inajitegemea yenyewe. Inatumika mara nyingi kama msaada. Imam Ali (a) anasema: “Haki ndio msaada wenye nguvu sana. Batili inategemea na vingine kuwepo. Inajaribu kujifunika yenyewe katika sura ya haki, na kuitumia ili kusaidiwa yenyewe na kuungwa mkono. Usemi wa hekima: Haki ni madhubuti, haitavunjika kama povu katika kuguswa tu. Laa, sivyo, unaweza ukaizungusha huku na huko kutwa nzima, lakini itakuwa kamili na nzima wakati wa jioni.
3. Haki wakati wote itaishinda batili, hata kama itachukua muda. Wale ambao hawana subira wala hekima ya kujua kwamba hatimae haya ndio yatakayokuwa matokeo, wanadanganywa na batili. Watu wenye hekima hata hivyo, huwa wanaridhia kusubiri. Wao wanajua kwamba mwisho wa yote haki itaibuka kuwa mshindi. Mwenyezi Mungu anasema katika Suratul-Anbiyaa: Bali tunaitupa haki juu ya batili ikaivunja na mara ikatoweka . . . (Q 21:18). Povu linaweza kuwa na nguvu kwa muda, lakini hatimae litatoweka. Waumini wanapaswa kuwa na imani na subira kujua kwamba hatimae wao, wakiwa upande wa haki, wataibuka washindi.
4. Wakati maji yanapotulia na kujimwaga kwenye maenao yaliyolala, povu hupungua na mara tu kutoweka. Kisha maji safi na halisi huonekana. Wakati binadamu wanapokuwa watulivu na wakawa tayari kuiona haki, ile batili iliyopo juu ya haki hupungua kisha hutoweka. Ndipo haki, pamoja na usai wake wote huja kutambulika na kukubalika.
Aya ya Qurani iliyopo hapo juu ni mfano mzuri wa jinsi mwanadamu anavyoweza kujifunza mengi kutoka kwenye maumbile. Ni kifungua macho kinachotukumbusha sisi kutembea kwenye mgongo wa ardhi kwa macho na masikio ya wazi kwa ajili ya kuelewa. Ni hasara kubwa kwetu endapo tutayapita masomo mazuri kama hayo ya maumbile, tukiyaangalia lakini kwa kweli bila kuyaelewa. Ndio maana Mwenyezi Mungu kila mara anatukumbusha sisi ndani ya Qurani Tukufu kutafakari juu ya maumbile: Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na kutofautiana usiku na mchana, ziko ishara kwa wenye akili. (Q 3:190).
Vyanzo: Ayatullah Naasir Makaarim Shirazi (mhariri), Al-Amthal fi Tafsiir Kitabillah; Muhammadi Rayshahri, Mizanul-Hikma.
Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo