إِنَّ اللَّـهَ لَا يَسْتَحْيِي أَن يَضْرِبَ مَثَلًا مَّا بَعُوضَةً فَمَا فَوْقَهَا ۚ
Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kupiga mfano wowote,
wa mbu au ulio zaidi yake . . .
(Sūratul Baqarah, Na.2, Āyah 26).
Mwenyezi Mungu Mtukufu anatoa mifano mingi ndani ya Qurani. Mifano hii inafanya mambo yawe rahisi kueleweka. Kwa mujibu wa aya hiyo hapo juu, mifano hii vilevile inatumika katika kutofautisha kati ya wale ambao wameongozwa sawasawa na wale ambao hawakuongozwa. Maudhui ya mfano huo yanabeba umuhimu ambao unavuka zaidi ya jambo la dhahiri linalozungumziwa katika aya hiyo.
Tafsiri ya aya hii inahitaji maelezo ya usuli (background) wake. Aya inazungumzia juu ya mwelekeo na tabia ya wanafiki. Moja ya mambo haya ya msingi nyuma ya unafiki ni kutafuta visingizio. Mnafiki anatafuta kisingizio au sababu ya kushutumu na kulaumu. Yeye mwenyewe hafanyi kitendo chochote ambacho kinastahili kusifiwa lakini wakati wote atakuwa anatafuta makosa kwenye vitendo vya wengine. Ayatullah Nasir Makarim Shirazi katika kitabu chake ‘Mithalhaye Zibaaye Quran’ (Mifano mizuri ya Qurani) anasema katika tafsiri ya aya hii kwamba kama jumuiya itajenga Kituo cha Kiislam ambacho kinajumuisha pamoja na msikiti, maktaba na nyumba za kuishi na kadhalika, basi mnafiki atalikosoa hilo na kusema kwamba pesa hizo zingeweza kutumika vizuri kwa kuwalisha wenye njaa ambao wanaishi ndani ya jumuiya hiyo. Kama mnafiki huyo huyo atakuwa ni mmojawapo miongoni wale wanaotumia mali kusaidia masikini na kuwalisha, angesisitiza kwamba pesa hizo zitumike katika kujenga kituo kwa ajili ya Uislamu ili kwamba uenezi wa maadui wa Uislamu uweze kukabiliwa. Mnafiki hana maoni thabiti juu ya jambo hilo. Anachokitaka tu ni kuwapinga wale wanaofanya kazi ambayo yeye mwenyewe hawezi kuifanya.
Wakati Mwenyezi Mungu aliposhusha aya fulani zenye mifano ndani yake, wao wanafiki walianza kutafuta makosa. Mwenyezi Mungu ni mkuu kuliko kwamba Yeye atoe mifano ya viumbe dhaifu na vidogo kama vile buibui na visubi (gnats), au vitu visivyokuwa na uhai kama vile moto, radi, na mwanga wa radi, wao walisema. Ujumbe wao wa kinyume na wenye kushuku ulikuwa ni kwamba aya kama hizo haziwezi kuwa zimetoka kwa Mwenyezi Mungu. Hata hivyo, kama aya hizo zingekuwa ni ngumu kueleweka na mifano ingekuwa ya vitu vyenye utata na vya dhahania tu, majibu yao yangekuwa kwamba hizi zinawezaje kuwa ni aya za Mwenyezi Mungu ambapo hatuwezi kutambua kitu chochote. Kwa nini Mwenyezi Mungu asiweze kuelezea haya mambo yenye utata katika njia nyepesi zaidi ili kila mtu aweze kuelewa? Upinzani kama huo ulipatikana miongoni mwa kaumu za Mitume wengine.
Mifano mizuri ni sehemu ya hotuba fasaha. Inavutia kwenye hadhira na inaweza kushusha mambo tatanishi na magumu kufikia kiwango cha msikilizaji. Ukubwa au nafasi ya mfano maalum hauna uhusiano na nafasi ya yule mwenye kutoa mfano huo. Badala yake, matumizi ya mfano unaofaa kulingana na mada na mazingira yanaonyesha uwezo wa msemaji. Msemaji mwenye kipaji ana uwezo wa kuvutia nadhari ya hadhira kupitia matumizi ya mifano inayovutia na kupendeza. Mifano inaweza kuwa ya kitu chochote, suala muhimu ni kufanya jambo kuwa wazi na la kueleweka zaidi. Ufasaha unajumuisha pamoja na uzuri wa lugha na kina cha maudhui vilevile. Aya za Qurani zina vyote hivyo, na mifano ya Qurani inaelezea aina hii ya ufasaha.
Vyanzo: Āyatullāh Nāsir Makārim Shirāzī, Mithalhaye Zibaye Quran – Jz.1.
Āyatullāh Nāsir Makārim Shirāzī – Al-Amthāl fī Tafsīr Kitābillāh
Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo