Tafakuri ya 8, Āyāt 16: 120 – 121: – Mfano wa Nabii Ibrahim (a)

إِنَّ إِبْرَ‌اهِيمَ كَانَ أُمَّةً قَانِتًا لِّلَّـهِ حَنِيفًا وَلَمْ يَكُ مِنَ الْمُشْرِ‌كِينَ ﴿١٢٠﴾ شَاكِرً‌ا لِّأَنْعُمِهِ ۚ
Hakika Ibrahim alikuwa ni umma, mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, mnyofu, wala hakuwa katika washirikina. Mwenye kuzishukuru neema Zake…..
(Suuratun Nahl, Na. 16, Aayaat :120-121)

Kifungu hiki cha maneno kinamtukutuza Nabii mtukufu Ibrahim (a), Mtume wa Mwenyezi Mungu na mkuu wa dini zenye kuamini Mungu Mmoja. Shaksia yake ni mvuto kwa waumini wote. Uaminifu wake, kutafuta kwake ukweli, msimamo wake thabiti dhidi ya washirikina, na uhusiano wake wa karibu na Mwenyezi Mungu, vyote vinachukua ushahidi juu ya tabia yake adhimu na ya mfano. Katika kifungu hiki cha maneno, Mwenyezi Mungu anaelezea sifa tano za Nabii Ibrahim (a) na matokeo matano ya sifa hizi.

Nabii Ibrahim (a) alikuwa:

1) Ni Taifa: Mtu mmoja, Ibrahim, hapa anazungumziwa kama ni Ummah mzima. Al-Amthal fi Tafsir Kitabillah inasema kwamba yafuatayo yanaweza kuwa ndio sababu zinazoweza kumfanya yeye kurejelewa kama taifa zima:

a) Shakhsia yake ilikuwa ni maarufu sana kiasi kwama ilikuwa ni sawa na ile ya kundi zima la watu. Miale ya utu wake ilikwenda mbali zaidi ya ile ya mtu mmoja.

b) Yeye alikuwa ni kiongozi na mwalimu wa binadamu. Wengine walimfuata yeye. Kama kiongozi, yeye alikuwa ndio msukumo au mvuto nyuma ya vitendo vyao vyote na hivyo akachukuliwa yeye binafsi kama taifa.

c) Yeye alikuwa ndiye muabudu Mungu mmoja peke yake wa wakati wake – taifa la tawhiid miongoni mwa taifa la waabudu masanamu.

d) Yeye alikuwa ndio asili na chanzo cha Ummah wa Kiislamu.

Hadithi moja ndani ya Safiinatul Bihaar kutoka kwa Ma’asuumiina (a) inasema kuhusu Abdul Muttalib ambaye pia alikuwa mtu maarufu: ‘Atafufuliwa Siku ya Kiyama kama taifa moja, juu yake itakuwepo hadhi ya Wafalme na sifa za Mitume.’

2) Mtiifu kwa Mwenyezi Mungu: Yeye alimtii Mwenyezi Mungu katika masuala yote.

3) Mnyofu: Neno Haniif linatumika kuonyesha ile njia ya kati na kati, isiyolemea kwenye upande wowote. Linazungumzia juu ya mtu ambaye anasimama wima akiwa amenyooka juu ya njia ya kati na iliyowekwa sawa ambayo ni sahihi. Neno hili limetumika zaidi ya mara sita ndani ya Qur’ani Tukufu kumuelezea Nabii Ibrahim (a) na itikadi yake.

4) Mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu: Nabii Ibrahim (a) alikuwa mwenye shukurani katika moyo na maana halisi wa neno lenyewe. Alikubali kwamba yote yale aliyokuwa nayo yalitoka kwa Mwenyezi Mungu na aliyatumia katika kumtumikia Mwenyezi Mungu. Matumizi sahihi ya fadhila alizojaalia Mwenyezi Mungu juu ya mja ni shukurani ya dhati.

5) Hakuwa miongoni mwa washirikina: Licha ya kuishi ndani ya jamii ya waabudu masanamu, Nabii Ibrahim (a) alijisalimisha kwa Mungu Mmoja wa Kweli. Aliwaamuru watu wake kukanusha ibada masanamu. Kuwathibitishia kwamba masanamu hayo hayakuwa na uwezo wa ama kuwadhuru wao au kuwafanyia wema wowote, aliyaharibu masanamu yote isipokuwa lile kubwa lao. Wakati alipoulizwa kuhusu hilo yeye aliwaambia wayaulize masanamu hayo – kama yataweza kuongea. Kwa uchungu wa watu hao, bado hawakuwa na majibu ya kumpa yeye. Qur’ani Tukufu inasema: Basi wakajirudi nafsi zao. Wakasema: Hakika ninyi ndio madhalimu. Kisha wakasimamia vichwa vyao. Wewe unajua kwamba hawa hawasemi (Q 21:64-65). Hii ilikuwa ndio njia yake ya kuwaonyesha watu uongo kamili wa imani zao.

Sifa nyingi kubwa kubwa zilijumuika ndani ya shakhsia ya Nabii Ibrahim (a). Aayatullaah Naasir Makaarim Shiraazii ndani ya Tafsiir yake juu ya fungu hili la maneno anamnukuu mshairi mmoja wa Kiarabu ambaye anasema:  “Haiko nje ya uwezo wa Mwenyezi Mungu kuujumuisha ulimwengu (sifa zote njema) ndani ya mtu mmoja.”

Chanzo: Āyatullāh Makārim Shirāzī, al-Amthāl fī Tafsīr Kitaballāh.

Tarjuma na: al-Haj Ramadhani S.K. Shemahimbo