Tafakuri ya 5, Āyat 33:5 – 46 : Wajibu wa Mtukufu Mtume (s)

Kwa tafakuri za Qurani zilizopita, bonyeza hapa
  
  ﴾يَاأَيُّهَاالنَّبِيُّإِنَّاأَرْ‌سَلْنَاكَشَاهِدًاوَمُبَشِّرً‌اوَنَذِيرً‌ا﴿٤٥﴾وَدَاعِيًاإِلَىاللَّـهِبِإِذْنِهِوَسِرَ‌اجًامُّنِيرً‌ا﴿٤٦

 Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekutuma uwe shahidi na mbashiri na muonyaji. Na mlinganiaji kwa Mwenyezi Mungu kwa idhini Yake, na taa iangazayo
(Sūratul AHzāb, Na. 33, Āyāt: 45-46)

 

Katika aya hii, Mwenyezi Mungu anaelezea sifa tano za Mtukufu Mtume (s).
1. Shahidi – Mtukufu Mtume (s) ni shahidi katika njia tofauti:

a) Wa ukweli wa ujumbe wake. Sifa zake tukufu na tabia yake isiyo na makosa (ma’asum) ni ushahidi wa Ukuu wa Mwenyezi Mungu, na wa ukweli wa ujumbe aliouleta.

b) Juu ya vitendo vya Ummah wake. Yeye anawaona na atatoa ushahidi katika Siku ya Kiyama. Baada ya Mtukufu Mtume (s) Maimam pia ni mashahidi juu ya Mashi’ah wao. Mwenyezi Mungu anasema ndani ya Qurani: Tendeni vitendo, Mwenyezi Mungu na Mtume Wake na walioamini wataviona….. (Q 9:105). Hadithi moja ya Imam al-Sādiq (a) inasema: ‘Vitendo vya waja wa Mwenyezi Mungu vinaonyeshwa kwa Mtukufu Mtume (s) kila asubuhi, vyema na viovu. Mtu mmoja alikuja kwa Imam Ali al-Ridhā (a) na akamuomba amuombee kwa vile alikuwa na matatizo. Imam akamwambia: Unadhani kwamba huwa sikuombei? Kwa kweli mimi ninaonyeshwa vitendo vyako kila asubuhi na usiku. Wakati mtu yule aliposhangaa, Imam akasema: Je, hujaisoma aya hiyo (ya hapo juu)? Kwa hakika waumini waliorejelewa kwenye aya hii ni Ali ibn Abi Talib (na Maimam kutokana na kizazi chake).

c) Juu ya Mitume wengine. Kila Mtume mnamo Siku ya Kiyama atatoa ushahidi juu ya ummah wake. Mtukufu Mtume (s) vilevile atatoa ushahidi juu ya Waislamu. Kwa mujibu wa aya ya Q 4:41: Mtukufu Mtume (s) pia atatoa ushahidi juu ya Mitume wengine. Basi itakuwaje tutakapowaletea kila ummah shahidi na tukakuleta kuwa shahidi juu ya hawa? Kwa kuwa yeye aliumbwa kabla ya Mtume mwingine yoyote, basi yeye ataletwa mbele kama shahidi juu yao wote.

2. Mbebaji (mbashiri) wa habari njema – yeye alitumwa kuja kuwapa habari njema wale wema na wachamungu, ambao wanajali na kumkumbuka Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Yeye anawaambia juu ya mafanikio na malipo, juu ya radhi ya Mola Wao, juu ya malipo yasiyoelezeka ambayo yanawasubiri. Wao kwa hiyo wanavutika kwenye wazo la thawabu (malipo).

3. Muonyaji (Nadhīri) – Mtukufu Mtume Muhammad (s) ametumwa kuja kuwaonya wale ambao hawaamini na wanaoikataa dini, wale ambao hawajali na hawajishughulishi, wanaozembea juu ya maisha yajayo. Anawaonya juu ya hasara watakayoipata jinsi maisha yanavyopita bure bure tu, juu ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu chungu iumizayo ambayo inawangojea wao. Wanadamu wana mapenzi ya kisilika ya kuepuka uovu kutoka kwenye nafsi zao wenyewe. Hili linawafanya wawe wenye kuvutika kuitikia ujumbe ambao unapiga mbiu dhidi ya madhara.

4. Anayelingania kuelekea kwa Mwenyezi Mungu (Dā‘ī ilallāh) – mara onyo na habari njema vinapokuwa vimetolewa, uwanja unakuwa umetayarishwa. Binadamu sasa ni mwenye kupokea kile Mtume atakachokisema. Kazi inayofuatia ni kuwaita wao kwenye ibada na utii wa Mwenyezi Mungu, kuwaonyesha njia ambayo wanapaswa kuipita, na kuwafundisha jinsi ya kuamiliana na jamii. Huu ni wajibu wa kuwaonyesha wanadamu njia ya kuelekea kwa Mwenyezi Mungu.

5. Taa yenye kutoa mwanga (Sirājul-Munīr) – Mtume anaangazia njia kwa ajili ya wengine kupitia mfano wake, na mafundisho anayoyahubiri. Kama Imam Ali (s) anavyosema: “Yeye ni taa ambayo mwanga wake unachoma, kimondo ambacho mwanga wake unang’ara na mwale ambao cheche zake ni angavu.” (Nahjul Balāgha, Hotuba ya 94). Wale ambao ni vipovu kiroho hawatauona mwanga huo, kama vile ambavyo kipofu wa kawaida asivyoweza kunufaika na mionzi ya  jua. Mwanga unatoa ukunjufu na faraja kwa mwanadamu; unachochea ukuaji  na unaendeleza mwondoko na shughuli. Kadhalika Mtume anatoa faraja kwa ajili ya waumini, mafundisho na maisha yake yanasababisha ukuaji wa kiroho, na ujumbe wake unakuza harakati na shughuli juu ya njia iliyonyooka. Bila ya yeye kuna giza la ujinga na ulafi.

Vyanzo: Āyatullāh Nāsir Makārim Shirāzī – Al-Amthāl fī Tafsīr Kitābillāh;
Aghā Muhsin Qarā’atī Kāshānī, Tafsīr-e Nūr